Nyota wetu
Aliyekuwa gwiji mcharaza gitaa maarufu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo 🇨🇩, Denis Lokassa Kasiya ,maarufu kama Lokassa ya Mbongo ,aliyefariki miezi sita iliopita,bado mwili wake haujazikwa.
Hii imesababisha kuzuka kwa sintofahamu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa mashabiki wake nchini mwake,barani Afrika ,Ulaya na Amerika.
Lokassa (80) ,ambaye alifariki katika Hospitali ya St Joseph ,Nashua,nchini Marekani ,machi 14, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mrefu ,alikuwa kiongozi wa bendi maarufu ya Soukous Stars ,iliokuwa na makao yake mjini Paris, Ufaransa.
Hapo awali,aliwahi kutamba na bendi ya Tabu Ley Rochereau ya Afrisa International na baadaye bendi ya All African Stars.
Kabla mauti haijamfika,alikuwa akipambana na ugonjwa wa kisukari na pia alikuwa akipata nafuu kutokana na kiharusi kidogo alichopata miaka michache iliopita.
Mtandao wa Taifa Leo umeripoti kuwa mwili wa mwananziki huyo ulirudishwa nyumbani Kinshasa, ambao ni mji mkuu wa DRC ,mnamo April ,na kwamba tangu wakati huo ,mwili huo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ,katika moja ya hospital jijini Kinshasa.
Baada ya mwili kuwasili,wakati huo ulipelekwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa N’Djili na wanamziki wenzake,familia, ndugu,mashabiki na viongozi wa Serikali.
Kwenye mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha Televisheni nchini humo,watoto wawili wa Lokassa walitoa wito kwa Serikali ya DRC ,kusaidia katika mipango ya maziko ya baba yao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kinshasa ,ilitarajiwa kuwa Wizara ya Utamaduni na Sanaa ingekuwa mstari wa Mbele katika mipabgo hiyo kama ilivyokuwa kwa magwiji wengine wa mziki wa DRC.
Akizungumza na Taifa leo hivi majuzi,mwanamziki wa Kinshasa,Lofombe Gode amesema bado haijafahamika iwapo familia yake au maofisa wa serikali wanafanya mipango yoyote ya maziko.
“Bado hakuna taarifa rasmi si tu kutoka kwa Serikali, bali hata kwa familia yake,zinazohusu maziko yake,maana sisi wote tunasubiri kutangazwa kwa tarehe husika”.