HABARI KUU
Kiongozi wa kanisa katoliki Duniani, Papa Francisco amewateuwa mapadri wawili kuwa maaskofu kwenye majimbo mawili ya kikatoliki ya Njombe na Bukoba.
Maaskofu hao wateule ni pamoja na; Padri Jovitus Mwijage kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba na Padri Eusebio Kyando kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe .
Katika taarifa iliochapishwa na Vatican inasema Papa Francisco amemteua Padri Eusebio Kyando kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa msimamizi wa kiroho wa jimbo hilo.
Jimbo Katoliki la Njombe limekuwa wazi kwa muda mrefu kufuatia kifo cha Mhashamu Askofu Alfred Maruma na kwa upande wa jimbo la Bukoba Mhashamu Askofu Desderius Rwoma alistaafu kwa mujibu wa sheria za kanisa katoliki.
Hii ni mara ya kwanza kwa kanisa katoliki kupata teuzi mbili za maaskofu kwa wakati mmoja kwa miaka ya hivi karibuni kutoka kwa Baba Mtakatifu.