HABARI KUU
Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameanzisha safari zisizohitaji visa kwa Waafrika wote ,na kuifanya Rwanda kuwa nchi ya 4 barani Afrika kufanya hivyo.
“Pia tumeondoa vizuizi vya visa kwa kila raia wa nchi ya Afrika pamoja na raia wa Mataifa mengine mengi . Mwafrika yeyote anaweza kupanda ndege na kuja Rwanda wakati wowote anaotaka na hatalipa kitu chochote kuingia nchini mwetu”
Amesema Rais Paul Kagame.
Aliongeza kwa kusema hatua hiyo inalenga kufaidisha soko la utalii barani Afrika linalokua likipigwa jeki na ukuaji wa uchumi wa kati barani humo.
Rwanda imekuwa kwenye mkakati mzito wa kuhakikisha inakuza utalii wake huku ikitumia vilabu kama Arsenal, Bayern Munich na PSG kujitangaza kama kivutio cha utalii.
Rwanda sasa inaungana na nchi kama Ushelisheli,Gambia,na Benin ambazo kwa muda sasa zimekuwa zikitoa visa huru kuingia kwenye nchi hizo.
Wiki hii, Rais wa Kenya William Ruto alitangaza kuwa nchi hiyo itamaliza masharti ya Visa kwa raia wote wa kiafrika ifikapo 2024.
Nchi kadhaa za Afrika zimeingia makubaliano baina ya nchi mbili za usafiri bila visa ,hivi karibuni Afrika kusini na Ghana,Uganda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.