HABARI KUU.
Tume ya utumishi ya Walimu Tanzania (TSC) imemsimamisha kazi Mwalimu Maganga Japhet kutokana na tuhuma za utoro kazini na kukaidi au kukataa kutekeleza maelekezo halali ya viongozi wake.
Taarifa za kusimamishwa kwa Mwalimu Maganga ambaye awali alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ,zimetolewa kupitia barua ya taarifa kwa umma iliyosainiwa na kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini wa Manispaa ya Temeke, Fransisca Mselemo.
Barua hiyo imeeleza kuwa ,Maganga amesimamishwa kazi na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya chini ya Tume ya utumishi wa walimu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya nidhamu ya walimu.
Taarifa hiyo imeeleza uamuzi wa kusimamishwa kazi Maganga , ulifikiwa Desemba 5,2023 ambapo kabla ya kusimamishwa ,Maganga alikuwa mwalimu wa shule ya Msingi Tandika iliyopo jijini Dar es salaam.
Awali, Maganga aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera na Rais Samia Suluhu Hassan ingawa ilielezwa kuwa Maganga alikataa uteuzi huo na kusalia Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).