MICHEZO
Ivory Coast imepanda nafasi 10 duniani kwenye msimamo wa viwango vya Fifa baada ya kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika, huku Nigeria waliofika fainali wakipanda nafasi 14.
Super Eagles sasa wapo nafasi ya 28 licha ya kupoteza mchezo wa fainali, na kuwafanya timu ya tatu bora kutoka Afrika yenye viwango vya juu duniani.
Ivory Coast imesogea hadi nafasi ya 39 duniani baada ya ushindi wa Afcon.
Angola ndio wamenufaika zaidi, baada ya kupanda nafasi 24 hadi namba 93, baada ya kutinga robo fainali.
Tanzania imepanda nafasi mbili hadi 119 duniani.
Morocco imesalia kuwa timu yenye viwango vya juu Afrika, ikipanda hadi nafasi ya 12, licha ya kuondolewa kwenye 16 bora, na Senegal wapo nafasi ya 17 baaada ya kutolewa kwenye raudi hiyo ya 16.
Tunisia na Algeria zimedondoka kwa nafasi 13, na kufikia 41 na 43, baada ya kutolewa kwenye ngazi ya makundi.
Washindi wa Kömbe la Dunia 2022, Argentina wapo kileleni wakifuatiwa na Ufaransa na England.