HABARI KUU
Wakosoaji nchini Kenya na Nigeria wameeleza wasiwasi wao juu ya idadi ya safari za nje zinazofanywa na ma-Rais wa nchi hizo William Ruto na Bola Tinubu.
Gazeti la The Standard la nchini Kenya limembatiza Rais Ruto jina la “Rais anayeruka” huku likisema kuwa pamoja na hali ngumu nchini, Rais huyo ameendelea kuzipa kipaumbele safari za nje.
Kwa upande wa Nigeria Kiongozi wa Upinzani Bw.Atiku Abubakar amesema kuwa nchi hiyo haihitaji Kiongozi ambaye ni “Mtalii Mkuu” anayesafiri sana nje huku nchi ikizama kwenye magumu.
Naye mchambuzi wa sera za mambo ya nje nchini Kenya Profesa Macharia Munene ameeleza kuwa baadhi ya safari zina umuhimu lakini zingine hazina umuhimu ni za kujitukuza.
Kampuni binafsi inayosimamia matumizi ya Serikali nchini Kenya imeeleza kuwa bajeti ya safari za ndani na nje imekuwa juu ukilinganisha na uongozi uliopita, na imeongezeka kwa asilimia 30 kulinganisha na matumizi ya mwaka jana.
Aidha ma-Rais hao pamoja na wasemaji wao wameeleza kuwa safari hizo si ubadhirifu bali ni moja ya hatua za kujaribu kuyatatua matatizo yaliyopo nchini.