MICHEZO
Kundi la Ramadhani Brothers kutoka Tanzania limepata ushindi wa kwanza wa America’s Got Talent: Fantasy League ambapo wamepewa zawadi ya $250,000 (shilingi milioni 636).
Fadhili Ramadhani na Ibrahim Jobu wameibuka washindi wakiwashinda washindani wengine ambao ni pamoja na Pack Drumline, V.Unbeatable, Sainted na Musa Motha.
“Ushindi huu una maana kubwa sana kwetu. Tuna furaha isiyoelezeka,” wameeleza na kuongeza kuwa watatumia sehemu ya fedha hizo kununua vifaa vya mazoezi kwa ajili ya wanamieleka wengine nchini Tanzania.
Ushindi huo ni matokeo ya safari ya miaka miwili ambapo awali walitarajia kushirikia hatua ya mchujo ya AGT Toleo la 17, lakini walikwama baada ya Jobu kutopata visa kwa wakati.
Kutokana na kuchelewa huko waliamua kushiriki mashindano mengine yakiwemo Australia’s Got Talent, Got Talent España na Românii au talent ambayo yaliwaandaa kushiriki AGT Toleo la 18.
Ramadhani Brothers waliwavutia majaji kwa kwa mazoezi yao ya sarakasi na kubebana kwa namna isiyo ya kawaida, lakini walishindwa na Adrian Stoica and Hurricane ambao waliibuka wa AGT Toleo la 18.
Wameeleza kuwa ilipofika wakati wa “Fantasy League” waliamini kwamba ni zamu yao kushinda kutokana na maandalizi waliyokuwa wamefanya, lengo ambalo wamelikamilisha.