HABARI KUU
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kuweka sharti kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwenye tafiti zozote nchini zinazohusisha masuala ya chakula na lishe katika Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo leo wakati wa ziara ya kukagua na kuona kazi zinazofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe kwa upande wa maabara iliyopo Mikocheni, Dar Es Salaam.
Amesema maabara hiyo ya chakula na lishe ni moja ya maabara kubwa na zinazoaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambapo amefurahishwa na kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuja na ushahidi wa kisayansi.
Maabara hiyo imegawanyika katika sehem tatu ambazo ni maabara ya chakula (food chemistry) ambayo inafanya uchunguzi wa viinilishe (macro and micro nutrients), maabara inayofanya uchunguzi wa viashiria vya viini lishe mwilini (micronuient biomarkers), na maabara inayofanya uchunguzi wa hali ya lishe (body composition) ikiwa ni pamoja na kugundua kama chakula kimeharibika.
Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya sukari na chumvi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa yamekuwa yakiongezeka kila siku.