HABARI KUU
Mbwa wa Rais wa Marekani Joe Biden aitwaye Commander aliwang’ata maafisa usalama kwenye matukio takriban 24, nyaraka zilizotolewa zimeonesha.
Taarifa za maafisa usalama zinaonesha kiwango ambacho mbwa huyo aina ya German Shepherd alivyosababisha sekeseke kwa walinzi wa Rais.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu amesema kung’atwa huko kulisababisha maafisa usalama kubadili mbinu zao kwa “kuweka nafasi kubwa” baina ya mbwa na maafisa.
Hatua hiyo ilikuja miezi kadhaa kabla ya Commander kuondolewa Ikulu ya White House.
Nyaraka hizo zimewekwa wazi kupitia sheria ya Uhuru wa kupata habari, baada ya maombi kuwasilishwa na taarifa kuwekwa mtandaoni.
Majina ya maafisa usalama yamefichwa na hata mbinu walizotumia kujilinda.
Nyaraka zilionesha matukio yasiyopungua 24 ya kung’atwa kati ya Oktoba 2022 na Julai 2023, ikiwemo taarifa ya maafisa usalama kung’atwa mikononi, kiunoni, kifuani, mapajani na mabegani.