HABARI KUU
Rais wa Urusi Vladimiri Putin amempa zawadi kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un gari la kifahari lililotengenezwa Urusi.
Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimesema gari hilo liliwasilishwa kwa wasaidizi waandamizi wa Bwana Kim siku ya Jumapili.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov baadaye alithibitisha kutolewa kwa zawadi hiyo akisema gari hilo aina ya Aurus, ni la kifahari kwa hali ya juu, aina ambayo inatumiwa na Bwana Putin mwenyewe.
Urusi na Korea Kaskazini, zimeunda uhusiano wa karibu tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.
Korea kaskazini inadhaniwa kuwa inaipa Urusi silaha kwa ajili ya vita, licha ya kuwepo na vikwazo vya kimataifa dhidi ya mataifa hayo mawili, limeripoti shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC. Mataifa hayo mawili yanakanusha kuvunja kanuni za vikwazo.
Bana Putin alimualika Bwana Kim katika eneo la Mashariki la Vostochny Cosmodrome mwezi Septemba mwaka jana, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Kim nje ya nchi katika kipindi cha miaka minne.