HABARI KUU
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, amesitisha likizo kwa watumishi wote wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) hadi hapo hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme itakapoimarika.
Dkt. Biteko amechukua hatua hiyo akiwa wilayani Kilombero, mara baada ya kutembelea mtambo wa kuzalisha umeme unaotumia maji wa Kidatu.
Amesisitiza kwamba kwa sasa watumishi wote wajikite kutafuta njia mbadala za kuimarisha nishati hiyo kwa wananchi.
Aidha amesema serikali inakusudia kuunda timu maalumu itakayoshirikisha Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kuongeza nguvu katika usimamizi wa rasilimali maji ambayo yanategemewa kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa umeme nchini.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema maelekezo hayo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati yatatekelezwa mara moja na kuwataka maofisa mabonde kuacha kukaa ofisini, badala yake watumie muda mwingi kufuatilia mienendo ya maji katika mabonde yao.