HABARI KUU
SERIKALI kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imetia saini mkataba mpya wa kibiashara wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 3.3 (sawa na Sh. Bilioni 8.3) kwa lengo la kuongeza huduma za mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Shirika la Burundi Backbone System (BBS) ya nchini Burundi.
Hafla ya kutia saini mkataba huo imefanyika leo Februari 23, 2024 jijini Dar es Salaam iliyoketi chini ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga na Mtendaji Mkuu wa BBS, Jeremie Hageringwe wakishuhudiwa na Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.
Baada ya tukio la kutia saini, Waziri Nape alisema uhusiano wa Tanzania na Burundi kupitia BBS ulianza 2019 wakati TTCL ilipotia saini mkataba wa awali wa kuwapa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Alisema mkataba huo ulihusisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa
Burundi-Burundi Backbone System kupitia eneo la Kabanga mpakani mwa Tanzania na
Burundi katika Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera na Manyovu upande wa Kigoma.
” Matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yamesababisha Serikali
ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo,” alisema na kuongeza kuwa mkataba mpya utaimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na utaboresha mawasiliano kati ya nchi hizi mbili.