HABARI KUU
Mahakama nchini Uganda imewahukumu zaidi ya wanawake 100 kifungo cha nje cha mwezi mmoja kila mmoja huku wakitakiwa kufanya kazi za kijamii baada ya kukiri kuwatuma watoto wao kuombaomba katika Jiji la Kampala.
Mahakama pia imepiga marufuku wanawake hao kurejea katika jiji hilo na kuamuru warudishwe katika wilaya wanakotokea ya Napak, Kaskazini mwa Uganda, gazeti la Daily Monitor limeripoti.
Baada ya kukiri makosa yao, wanawake hao waliomba kuhurumiwa, huku wengine wakisema ni wajane na wengine wakisema hawana waume.
“Nimesikiliza kilio chao na kuona hukumu ya kuwatupa jela haitakuwa sawa. Lakini ni lazima nitekeleze adhabu ili kukomesha hii tabia… Nikawapa adhabu ya kufanya kazi za kijamii bila kulipwa. Watatumikia adhabu hiyo kwa mwezi mmoja,” hakimu aliyesikiliza kesi dhidi ya wanawake hao, Edgar Karakire, ameliambia Daily Monitor.
Kutuma watoto kuombaomba ni kinyume na sheria za ulinzi wa watoto za Uganda na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha miezi sita au zaidi.