MAKALA
Hakuna cheo kinachoitwa RPC wala OCD wala OCS katika jeshi la polisi. Watu wengi hudhani ‘RPC’ ni cheo kinachomuwakilisha Kamanda wa Polisi wa mkoa, na ‘OCD’ ni cheo cha Kamanda wa polisi wa wilaya. Ni makosa. Hivi si vyeo, ni madaraka. Cheo ni ‘rank’ya kijeshi, madaraka ni majukumu ambayo askari anapangiwa.
Askari mwenye cheo kuanzia Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuendelea, anaweza kushika madaraka ya Kamanda wa polisi wa mkoa (RPC). Na mtu mwenye cheo kuanzia Mrakibu wa Polisi (SP) na kuendelea anaweza kushika madaraka ya Kamanda wa polisi wa wilaya (OCD).
Katika mfumo wa vyeo vya polisi, ambao nchi zote za Jumuiya ya madola hutumia (tumerithi kutoka kwa Wakoloni, Uingereza) kuna vyeo vya maafisa na visivyo vya maafisa. Vyeo visivyo maafisa ni Konstebo, Koplo, Sajenti na staff Sajenti.
Kwa upande wa Maafisa anaanza Mkaguzi msaidizi wa Polisi (Assistant Inspector), kisha Mkaguzi wa Polisi (Inspector), kisha Mrakibu msaidizi wa polisi (ASP), anafuata Mrakibu wa polisi (SP), kisha Mrakibu Mwandamizi wa polisi (SSP). Hawa hupandishwa vyeo kwa kusomea kozi maalumu, na baadae huthibitishwa na Tume ya utumishi ya Polisi.
Baada ya hapo wanafuata makamishna, na wa chini kabisa ni Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP), anafuata Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), anafuata Naibu Kamishna (DCP), anafuata Kamishna (CP), kisha IGP. Hawa wako kwenye mamlaka ya uteuzi ya Rais. Yeye pekee ndiye huamua kumpandisha afisa wa polisi kutoka ACP kwenda SACP, au SACP kuwa DCP etc.
Hivi ndio vyeo vya polisi. Nadhani hapo hamjaona ‘RPC’wala ‘OCD’. Kama nilivyotangulia kusema awali hayo ni madaraka, sio vyeo. Kuna madaraka ya aina nyingi ndani ya jeshi la polisi kama vile mkuu wa kituo (OCS), Mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID), Mkuu wa upelelezi wa mkoa (RCO), Mkuu wa polisi wilaya (OCD), Mkuu wa polisi mkoa (RPC), Mkuu wa usalama barabarani wa mkoa (RTO), etc.
Kwa kawaida madaraka huendana na cheo. Kwa mfano mtu mwenye cheo kuanzia Mkaguzi wa polisi (Inspector) anaweza kupewa madaraka ya kuwa mkuu wa kituo cha polisi (OCS). Na mtu mwenye cheo cha Mrakibu wa Polisi (SP) anaweza kupewa madaraka ya kuwa Mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID), au Mkuu wa polisi wilaya (OCD) etc. Na mtu mwenye cheo kuanzia Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) anaweza kupewa madaraka ya kuwa mkuu wa polisi wa mkoa (RPC), Mkuu wa upelelezi wa mkoa (RCO), au madaraka mengine.
Kwa mfano mwaka jana ACP Stanley Kulyamo alitolewa kuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Geita kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara. Hii ina maana aliongezewa madaraka lakini cheo chake kilibaki kilekile cha ACP.
Hata hivyo inawezekana mtu mwenye cheo kikubwa akapewa madaraka madogo na mwenye cheo kidogo akapewa madaraka makubwa, japokuwa hutokea kwa nadra sana. Kwa mfano mwaka 2017, wakati SACP Lazaro Mambosasa anahamishiwa Kanda Maalumu ya Dar, alimkuta Mkuu wa Operesheni wa Kanda hiyo ni DCP Lucas Mkondya (ambaye aliwahi kukaimu ukuu wa polisi kanda maalum).
Kwahiyo kimadaraka SACP Mambosasa alikua “boss” wa DCP Mkondya. Lakini kwa cheo Mkondya alikua mkubwa kuliko Mambosasa. Kwahiyo kila walipokutana Mambosasa alilazimika kumpigia saluti Mkondya kabla ya kumpangia kazi (kwa sababu kinachopigiwa saluti ni cheo, si madaraka). Lakini kwa busara za IGP, akamhamisha DCP Mkondya na kumpeleka Mtwara kuwa RPC huko, ili kuepusha mgongano wa kimaslahi.
Watu pia wamekuwa wakichanganya ASP na ACP. ASP ni mrakibu msaidizi wa Polisi (Assistant Superitendent of Police). Ni cheo kinachofuatia baada ya Inspekta wa Polisi kama nilivyoeleza hapo juu. Mara nyingi ASP wengi huwa Wakuu wa vituo vya Polisi (OCS) au wakuu wa upelezi wa wilaya (OC-CID) au wakuu wa usalama barabarani wa wilaya (DTO) au mikoa (RTO).
Lakini ACP ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (Assistant Commisioner of Police). Ni cheo kinachofuata baada ya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) na ni cheo cha chini kabla ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi (SACP). Kwa kawaida ACP wengi ni Makamanda wa Polisi wa Mikoa (RPC), wakuu wa upelelezi wa mikoa (RCO) etc.