HABARI KUU
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikiria Venance Patrick Ngonyani (28) Mkazi wa mtaa wa Mahenge, anayetuhumiwa kumuua Hussein Mohammed Anafı (21) Kondakta wa Daladala yenye namba za usajili T.332 BXR TOWN ACE, wakati wakidaiana Shilingi 100 ikiwa ni sehemu ya nauli katika Daladala hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Marco G. Chilya amesema kuwa tukio limetokea Febuari 25, 2024 majira ya saa 12 jioni maeneo ya Mkuzo stendi iliyopo kata ya Msamala Manispaa ya Songea, ambapo marehemu alikuwa kwenye Gari ambayo alikuwa akifanyia kazi, Mtuhumiwa alipanda Gari hiyo kama abiria wengine na wakati wa kudaiwa nauli Mtuhumiwa alilipa nauli pungufu ya Shilingi 500/= badala ya 600/= ambapo kilichopelekea marehemu kumtaka Mtuhumiwa kulipa nauli stahiki kitendo ambacho kilisababisha malumbano na ugomvi baina yao ndipo Mtuhumiwa alipochomoa kisu alichokuwa kakificha kiunoni na kumchoma shingoni na kumsababishia kifo Kondakta huyo.
Aidha kamanda Chilya ametoa wito kwa Wananchi wote mkoani Ruvuma kuachia tabia ya kujichukulia sheria Mkononi.