HABARI KUU
Kijana mwenye umri wa miaka 25 amevunjika mkono Jumamosi usiku baada ya kuruka kutoka ghorofa ya nne huko Embu Town, nchini Kenya.
Kijana huyo ambaye polisi wamemtaja kwa jina la Daniel Mwinzi inaripotiwa kuwa alikwenda kumtembelea rafiki yake wa kike na tukio hilo likatokea.
Chifu wa eneo hilo Sammy Njagi, alithibitisha kisa hicho, akibainisha kuwa alipokea simu kutoka kwa mpangaji anayeishi katika ghorofa hiyo muda wa saa kumi na mbili asubuhi akimjulisha kuwa kuna mtu ameruka kutoka kwenye jengo hilo.
“Nilitembelea eneo la tukio na kumkuta mwanaume huyo ambaye niliweza kumtambua jina lake akiwa amejikunja kwa maumivu na kuushika mkono wake wa kushoto. Inaonekana alikuwa amevunjika,” alisema Chifu.
Kulingana na ripoti mbalimbali ikiwemo ya Citizen TV, mwanaume huyo inasemekana kuwa huenda alikua akijaribu kutoroka kutoka kwa nyumba ya mwanamke huyo.
Mwanaume huyo anadaiwa kupanda ngazi zinazoelekea kwenye balcony, kabla ya kuruka kwa kasi kuelekea chini.
“Mwanaume huyo alikuwa na mwanamke ambaye walicheza naye usiku wa kuamkia jana kwenye klabu ya usiku iliyo karibu. Haijabainika kwa nini aliruka,” alisema Chifu.
Polisi kutoka Embu walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye, na kumpeleka mtu aliyejeruhiwa katika hospitali ya Embu Level Five ambako anaendelea kupata nafuu.
Polisi wamemhoji mwanamke huyo anayesemekana kuwa mmiliki wa nyumba hiyo na bado tunasubiri kupata maelezo zaidi ya kile kilichojiri ndani ya nyumba mpaka kupelekea kijana huyo kujitosa na kuvunjika mkono.