HABARI KUU
Habari zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa kundi la waendesha bodaboda, leo Februari 27, 2024 wamelichoma moto na kuliteketeza basi linalodaiwa kuwa ni mali ya Kampuni ya Saibaba, lililokuwa linatoka jijini Dar es Salaam kuelekea Arusha, baada ya kudaiwa kumgonga bodaboda mmoja na kusababisha kifo chake.
Habari zilizotufikia hivi punde, zimeeleza kuwa tukio hilo limetokea katika eneo la Kona ya Semkiwa, Korogwe mkoani Tanga na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya pande mbili za barabara hiyo, jambo lililosababisha foleni iliyodumu kwa takribani saa mbili.
Kwa mujibu wa mashuhuda, baada ya ajali iliyosababisha kifo cha mwendesha bodaboda, wenzake walijikusanya na kulizingira basi hilo, wakawaamuru abiria wote kushuka na kushusha mizigo yao kabla ya kuliteketeza kwa moto.