MICHEZO
Kocha Mkuu wa Real Madrid Carlo Ancelotti amekiri ni vigumu kumuacha Luka Modric kwenye benchi baada ya kiungo huyo mkongwe kufunga bao zuri katika ushindi wa 1-0 wa Real Madrid dhidi ya Sevilla mwishoni mwa juma lililopita.
Modric mwenye umri wa miaka 38 ambaye ameanza mechi 11 pekee za ligi msimu huu aliingizwa kutoka benchi katika dakika ya 75 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu na akafunga bao kwa shuti la mbali dakika sita tu baada ya kuingia.
Mkataba wa mchezaji huyo wa Kimataifa wa Croatia unatarajiwa kumalizika msimu huu wa majira ya joto, na kukosa muda wa kucheza msimu huu kumesababisha uvumi kuwa anaweza kuchagua kuhama baada ya miaka 12 ya kukaa na Madrid.
Ancelotti amesema kuwa Modric, Toni Kroos pamoja na Nacho Fernandez, ambao mikataba yao pia inakamilika msimu huu wa majira ya joto wamepata haki ya kuamua mustakabali wao wenyewe.
“Modric, Kroos, Nacho wote wako katika hali moja,” alisema Ancelotti.
“Siingilii katika hilo, Klabu ina muda wa kutatua hayo yote miezi michache ijayo.. kutokana na heshima niliyonayo kwa Modric siwezi kumpa ushauri, ana akili sana, anajua vizuri kabisa kile anachopaswa kufanya.”
Modric ameshinda mataji 24 akiwa na Madrid yakiwamo matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini anakabiliwa na ushindani ulioongezeka katika safu ya kiungo msimu huu kutoka kwa vijana Jude Bellingham, Eduardo Camavinga, Fede Valverde na Aurelien Tchouameni, pamoja na Kroos, ambaye amekuwa katika kiwango bora.