HABARI KUU
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kufanikiwa kwa jaribio la safari ya treni ya SGR kutoka Dar es salaam hadi Morogoro leo ni jambo la kujivunia kwa Watanzania kwani safari za majaribio kama hizo mara ya mwisho zilifanyika miaka 100 iliyopita na Wajerumani na kwamba sasa kilichobaki ni safari kuanza hiyo July ambapo nauli zitakazotumika zitatangazwa na LATRA hivi karibuni.
Akiongea Morogoro leo, Kadogosa amesema “Ni jambo la kujivunia kwa Watanzania, ni mafanikio makubwa kwa Taifa letu ujue safari kama hizi za kufanya majaribio zilifanyika miaka 100 iliyopita na Wajerumani lakini sasa hivi hapa Wataalamu 95% ni Watanzania ni jambo zuri kwamba Watanzania mnaweza kusimamia jambo kama hili na likafanikiwa”
“Tunamshukuru Mh. Rais ujue unapoona ujenzi unaendelea ni kwasababu kuna pesa zinatolewa, na pesa zinatafutwa , Rais unapomuona ana safiri ndio matokeo yake haya kwasababu kila mmoja anaweza akazungumza anavyotaka, Mh. Rais anahangaika sana kuhakikisha vipande vina Wajenzi, yametolewa maagizo na Rais inatakiwa mwishoni mwa July iwe imeanza kwahiyo sisi ratiba iko palepale”
“Kuhusu bei sisi kama TRC tulishapeleka lakini LATRA ana nafasi yake anaifanyia kazi kuna mahali anapitisha ndani ya Serikali na baadaye atatangaza, kwa mujibu wa sheria Mkurugenzi wa LATRA ndiye anatakiwa kutangaza”