HABARI KUU
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezindua Ofisi ya Shirikisho la Wamachinga na Bodaboda iliyojengwa mjini Babati itayokuwa mahsusi kwa makundi hayo katika kufanya vikao, mijadala na kutatua changamoto mbalimbali, zinazowakabili na kuwataka wasijishushe kwani hadhi yao ni kubwa.
Akizindua ofisi hiyo, Sendiga amesema, uwepo wa ofisi hii ni maono ya Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kwamba kila kundi lazima lifikiwe na litengenezewe mazingira mazuri ya kufanya kazi, ili waweze kuwa wazalishaji wazuri.
Amesema, ofisi hiyo imejengwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43, ikiwa na umeme, maji pamoja na samani, ambapo fedha hizo ni kutoka Serikali kuu, mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na michango ya wadau mbalimbali.
Sendiga pia amewataka Wamachinga pamoja na Bodaboda kutojichukulia kawaida kwani wao ni watu muhimu katika kusaidia upatikanaji wa kodi ambayo inakwenda katika shughuli mbalimbali za kiuchumi katika nchi yao.
“na Serikali inategemea kodi katika uboreshaji wa huduma za Afya, Elimu, Maji, Miundombinu n.k. Kwahiyo hapo ulipo jipigepige kifuani sema kuanzia leo sijichukulii poa,” aliongeza mkuu wa Mkoa Sendiga.
Kabla ya kufanya ufunguzi wa ofisi hiyo, Sendiga amemuahidi Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange kuwa ataleta Kompyuta mbili katika ofisi hiyo ya wamachinga na Boda Boda, ili kuwawezesha kufanya Biashara zao kidijitali.
“Muwaangalie wafanyabiashara wadogo wadogo wa China, India wanafanyaje Biashara zao”. Aliongezea Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu wa mkoa ametembelea na shule ya sekondari Kololi iliyopo Katika Kata ya Maisaka na Pauline Gekul iliyopo katika Kata ya Bonga, kuona mwenendo wa ukamilishaji wa baadhi ya Majengo ya shule hizo na kutoa maagizo ya ukamilishwaji wa haraka kwa majengo hayo ambayo baadhi ni vyoo vya wanafunzi, majengo ya Maabara za TEHAMA.