HABARI KUU
MJANE wa marehemu Harry Roy Veevers, raia wa Uingereza aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa nchini Kenya na binti zake wawili, wamepinga mahakamani ombi la watoto wengine wa marehemu kuuondoa mwili wa baba yao katika mochwari ya Mombasa ili wakauzike nchini Uingereza.
Parveen Din na binti zake wawili, Hellen Veevers na Alexandra Veevers, wamepinga pia shinikizo la kaka hao wawili ambao mama yao ni mwingine, wanaotaka mahakama iamuru kufanyika upya kwa uchunguzi wa kifo cha baba yao.
Richard John na Philip David Veevers wamekuwa wakitaka mwili wa baba yao ukafanyiwe uchunguzi mara tu utakapowasili Uingereza.
Lakini kupitia kwa wakili Mogaka Omwenga, mjane huyo na binti zake wameshikilia kuwa mahakama ya hakimu mkazi iliendesha kesi ya uchunguzi wa kifo cha tajiri huyo kwa haki.
Veevers alifariki dunia Februari 14, 2013, mjini Mombasa lakini tajiri huyo ambaye hakuacha wosia hajazikwa kutokana na mzozo wa mgawanyo wa mali zake kutokamilika.
Richard na Philip wamekuwa wakishuku kuwa dada zao hao wanaokutana kwa baba, Alexandra na Hellen kwa kushirikiana na mama yao Din, walihusika na kifo cha baba yao. Hata hivyo, uchunguzi uliochukuwa miaka 10 ulihitimisha kuwa, hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa mahamkamani kuhusisha mtu yeyote na kifo cha tajiri huyo.