HABARI KUU
Hatimaye Kampuni ya Ndege Tanzania kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake Injinia Ladislaus Matindi wametolea ufafanuzi hitilafu ya Ndege ya Shirika hilo iliyosababisha kutoka moshi ikiwa angani ikitokea Dar es salaam kuelekea Mbeya na kusababisha Marubani waigeuze na kurudi Dar es salaam.
Injiania Matindi leo ameeleza kuwa tarehe 24 Februari 2024, Jumamosi, Ndege hiyo ya Airbus A220-300 namba TC106 ilipata hitilafu kwenye injini yake moja baada ya kuruka kwa muda wa takribani dakika 30 ikiwa ni hitilafu iliyotokana na injini moja kupata joto na kusababisha moshi wa mafuta kuingia ndani ya ndege kupitia mfumo wa Air conditioner kwa muda wa dakika 5 kabla ya Marubani kuzima injini hiyo yenye hitilafu na moshi ukatoweka.
Matindi ameongeza kuwa kwa muda ambao Ndege ilisharuka kijiografia ilikua imefika maeneo ya Mbuga ya Hifadhi ya Mikumi ambapo baada ya kuzimwa kwa injini…. ndege ingeweza kuendelea na safari kwa kutumia injini moja lakini kwa kuzingatia kipaumbele cha usalama kwanza, Rubani Kiongozi Michael Lengaram aliamua kuirejesha Dar es salaam ikiwa ndicho kiwanja kilichokua karibu chenye uwezo wa kuipokea ndege hiyo ya A220.
Amesema tukio zima lilichukua takribani dakika 60 tangu ndege kupaa angani hadi kurejea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na sio masaa matatu au matano kama baadhi walivyosema mitandaoni ambapo amesisitiza kuwa katika tukio hilo hakukuwa na moto uliowaka wala Abiria aliyeonesha uhitaji wa vifaa saidizi vya upumuaji au kupoteza fahamu kama inavyoripotiwa na baadhi ya Vyombo vya habari.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Ubora Emmanuel Tivai alisema tatizo lililotokea ni la kawaida kiufundi hivyo hushughulikiwa kwa kufuata taratibu zinazotambulika kitaifa na kimataifa lakini inapohitajika taarifa kutolewa kwa Umma Taasisi haizuiwi kufanya hivyo.
“Katika tukio hili Wahudumu wa ndani ya ndege kwa kushirikiana na Marubani walichukua hatua za kwanza za kiusalama kwa Abiria ikiwemo kutoa taarifa sahihi kuhusu changamoto iliyojitokeza kuwa inadhibitika ambapo baada ya Wahudumu hao kuendelea kufanya kazi yao kwa uweledi mkubwa hofu waliyokuwanayo Abiria ilitoweka, kwa kuwa Ndege hii ina injini mbili hata baada ya kuzimwa kwa injini moja bado ndege hiyo iliweza kutua kwa usalama” – Tivai.
Ndege iliyopata hitilafu ilikuwa na Abiria 122 ambapo baada ya kurejea Dar es salaam abiria 104 walichagua kuendelea na safari huku Abiria 18 wakichagua kubadilishiwa tarehe za safari yao.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.