MICHEZO
Rais wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ Javier Tebas anataka Mshambuliaji wa Manchester United, Mason Greenwood abaki nchini humo mara baada ya mkopo wake wa msimu mzima katika klabu ya Getafe utakapomalizika.
Greenwood mwenye umri wa miaka 22, alijiunga na kikosi cha Madrid akitokea United Septemba mwaka jana baada ya mshambuliaji huyo wa zamani wa England kuachana na klabu yake ya zamani kufuatia uchunguzi wa uhalifu kuhusu uwezekano wa kujaribu kubaka.
Mashtaka dhidi ya Greenwood yalitupiliwa mbali, lakini aliihama klabu hiyo kufuatia uchunguzi wa ndani.
“Yeye (Greenwood) anaendelea vizuri kama mchezaji na ninatumani ataendelea kubakia katika soka la Hispania,” alisema Tebas akiwaambia waandishi wa habari mjini London. “Hiyo ni nzuri kwetu.”
Greenwood, ambaye amefunga mabao matano na kutengeneza mengine matano katika mechi 25 alizochezea Getafe, ana mkataba na United hadi Juni 2025.
Mmiliki mwenza mpya wa United, Sir Jim Ratcliffe hivi karibuni aliulizwa kuhusu Greenwood na kusema: “Tunahitaji kuangalia ukweli, kuhukumu kwa haki na kuzingatia maadili ya klabu ni nini. Kisha tunatoka katika hilo na uamuzi. Kwa sasa haifai kwangu kutoa maoni juu ya Mason Greenwood. “
Tebas ambaye kitaalamu ni mwanasheria, alisema hana nia ya kumhukumu Greenwood kwa sababu “hajahukumiwa” na mahakama.
“Unapaswa kuheshimu mchakato wa kisheria,” alisema Tebas.
“Watu wanaweza kuwa wanamhukumu kwenye vyombo vya habari, lakini unapaswa kuheshimu uamuzi wa kisheria. Hakuna kitu kingine cha kuzungumza juu yake. Hakuhukumiwa na maana yake hakupatikana na hatia.”