MICHEZO
Mama wa Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Kylian Mbappe ameripotiwa kuanza kutafuta nyumba huko Hispania ili kujiandaa kabla ya mwanaye hajakwenda kujiunga na Real Madrid.
Mshambuliaji huyo atamaliza mkataba wake na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu 2023/24.
Kinachoaminika ni kwamba mchezaji huyo atakwenda kujiunga na Real Madrid bure kabisa, licha ya kwamba bado kuna baadhi ya mambo hayajakamilishwa.
Licha ya kwamba kiufundi atakuwa mchezaji wa bure, lakini ukweli ni kwamba kunasa saini ya Mbappe si rahisi kiasi hicho.
Kinachoelezwa ni kwamba Mbappe atakwenda kulipwa pesa nyingi kuzidi usajili wa Jude Bellingham wa Pauni 114 milioni kama ada ya uhamisho na bonasi ya usajili.
Mbappe anaripotiwa kwamba alitoa masharti matatu ya kuhusu mkwanja ili akamilishe uhamisho wake.
Na kinachoelezwa ni kwamba Mbappe amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano huko Bernabeu.
Huku kingine ni kwamba Real Madrid itamsajili mdogo wake Mbappe, Ethan mwenye umri wa miaka 17, ili kufanikiwa kumshawishi mchezaji huyo aende kujiunga na timu yake.
Kundi la mawakala wanaomsimamia Mbappe, ambao wanasimamiwa na mama wa mchezaji huyo, mrembo Fayza Lamari, alikuwa na ombi hilo maalumu ambalo lilikubaliwa na raisi wa Los Blancos, Florentino Perez.
Na sasa ripoti kutoka Hispania zinafichua mama wa staa huyo, mrembo Fayza yupo Madrid kutafuta nyumba kwa ajili ya kwenda kuishi na mtoto wake wakati atakapotua kukipiga Los Blancos.
Madrid inajiandaa kumpa Mbappe Pauni 85.5 milioni kama ada ya usajili wakati atakapojiunga timu hiyo na kwamba atakwenda kuwa mehezaji atakayekuwa analipwa mshahara mkubwa kumzidi Bellingham.