NYOTA WETU
Mrembo wa Tanzania, Halima Kopwe ameingia katika kumi bora kwenye kipengele cha ushindani cha ‘Beauty with Purpose Project’ kwenye shindano la ulimbwende la dunia (Miss World) linaloendelea nchini India.
Hili ni Shindano la Urembo la Dunia la 71 ambalo limeanza Februari 18, 2024 na litahitimishwa Machi 09, 2024.
Kampeni ya Halima iliyoshida ni ‘Damu Yangu, Kizazi Changu’ ambayo ni mradi unaolenga kuboresha afya ya wanawake wajawazito na watoto nchini Tanzania na kusaidia kupunguza viwango vya vifo vya kina mama na watoto.
Lengo kuu la kampeni yake ni kushughulikia suala la vifo vya kina mama vinavyosababishwa na kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua na upungufu wa damu kwa watoto wachanga. Mradi huu, pamoja na mambo mengine, unajumuisha kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa kuchangia damu na kuandaa matukio ya uchangiaji damu kwa ushirikiano na kituo cha kitaifa cha Damu Salama na wadau wengine.
Zaidi ya hayo, mradi unalenga kukusanya fedha ili kusaidia vifaa vya matibabu na mahitaji mengine hospitalini kwa ajili ya uzazi salama, pamoja na kutoa bima ya afya kwa watoto wanaohitaji.
Halikadhalika, kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT, mradi unalenga kufikia wajawazito walio katika hatari kubwa ya uzazi na kuhakikisha kuwa wanajifungua salama watoto wenye afya njema.