MICHEZO
Mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi Cody Gakpo amefichua kuwa alifanya mazungumzo na Manchester United kuhusu uhamisho wa msimu wa majira ya joto wa 2022, lakini kuhamia kwake Liverpool msimu wa baridi mwaka uliofuata kwa kusema ulikuwa uamuzi bora kwake.
Mshambuliaji huyo mwenye uwezo mwingi alifurahia miaka mitano katika kikosi cha kwanza cha PSV Eindhoven kabla ya kusajiliwa na wekundu hao Januari 2023.
Wakati wa Erik ten Hag akianza kuinoa United, Gakpo alifanya mazungumzo naye kuhusu kuhamia Old Trafford, lakini hatimaye makubaliano hayakuweza kukamilika.
Gakpo alibaki PSV hadi dirisha la majira ya baridi na kisha akajiunga na Liverpool kwa dau la awali la Pauni Milioni 35.4.
Katika mahojiano na Sky Sports, Gakpo alifunguka juu ya ukubwa wa mazungumzo haya ya uhamisho na Man Utd na jinsi ilivyokuwa bora kwake kubaki na kusubiri kutua Liverpool.
“Tulikuwa majira ya joto kabla ya kujiunga na Liverpool. Nilikuwa nikiwasiliana na klabu (United) na kocha yeye ni Mholanzi kwa hivyo nilizungumza naye pia,” alisema Gakpo.
“Mwisho wa siku ilishindikana, na wakati wa majira ya baridi Liverpool ilikuja. Ulikuwa uamuzi bora kwangu.”