MAKALA
BILIONEA Jeff Bezos amerejea kwenye usukani wa ukwasi Duniani baada ya kuchukua nafasi ya kwanza katika orodha ya matajiri duniani akimpita Elon Musk. Bosi huyo wa Amazon ana utajiri wa Dola bilioni 200, akifuatiwa na Musk kwenye ukwasi wa Dola bilioni 198.
Kwa mujibu wa ripoti ya Bloomberg, Musk alipoteza takriban Dola bilioni 31 mwaka uliopita, wakati Bezos akipata Dola bilioni 23. Hisa za kampuni ya Tesla ya Musk zimepungua zaidi ya 7%.
Musk alichukuwa nafasi ya kwanza mnamo Mei 2023, akimshinda Mkurugenzi Mtendaji wa LVMH (LVMHF) Bernard Arnault, ambaye anaendesha moja ya kampuni kubwa zaidi duniani na inajumuisha chapa kama vile Louis Vuitton, Dior na Celine.
Mamilionea hao watatu Musk, Arnault na Bezos wamekuwa wakishindana kila mmoja kwa nafasi ya kwanza kwa miezi kadhaa.
Mapema mwaka huu, Jaji wa Mahakama ya jimbo la Delaware alitupilia mbali malipo ya Musk ya 2018 yenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 50 ambayo yalisaidia kumfanya kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi ulimwenguni.