NYOTA WETU
Kwa mara nyingine tena Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, alimuomba Msaidizi wake kumsomea somo la katekisimu wakati wa misa ya Jumatano.
Papa aliongoza misa hiyo ya kila wiki ambayo kwa mara ya kwanza ndani ya mwaka huu ilifanyikia nje katika uwanja wa St.Peters.
Kiongozi huyo pia alionekana kushindwa kupanda ngazi chache na kutoweza kurudi kwenye gari lake maalumu bila msaada kwani bado matatizo ya mfumo wa upumuaji na shida ya kutembea vinaendelea kumsumbua.
Jumatano iliyopita, Papa Francis alipelekwa hospitali kwa vipimo ambavyo havikutajwa na hadi sasa matokeo ya vipimo hivyo hayajawekwa wazi.
Katika kipindi hiki cha baridi barani Ulaya Papa amekuwa akiugua mara kwa mara kwa kile ambacho yeye mwenyewe pamoja na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican imekitaja kuwa ni kikohozi, mafua na shida kwenye mfumo wa upumuaji.