HABARI KUU
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamewasilisha salamu za rambirambi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi katika Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo lililoanza tarehe 10 Machi 2024 jijini Luanda, Angola
Wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Waziri wa Mambo Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Balozi Tete António pamoja na Mawaziri wengine wa nchi za SADC walitoa salamu hizo na kusifu uongozi mahiri na mchango wa Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na Kanda ya SADC hususan pindi alipokuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Jukwaa ya Uratibu wa masuala ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1989 – 1990 na pia aliongoza mchakato wa kubadili Jukwaa hilo kuwa SADC.
Kwa muda wa siku mbili, Baraza hili litajikita kupitia, kujadili na kuridhia Bajeti ya SADC kwa mwaka wa fedha wa 2024/25. Vile vile, Baraza litajadili hatua iliyofikiwa katika kugharamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC wa 2020–2030, Taarifa ya Kamati ya Rasilimali Watu na Utawala na hatua iliyofikiwa katika kutafsiri nyaraka muhimu za SADC kwa lugha ya Kiswahili.
Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Baraza la Mawaziri la SADC umeongozwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Ali Suleiman Ameir na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali.