HABARI KUU
Mkazi wa Kijiji cha Mashese, Daines Paul Mwashambo (30), ambaye alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kuwaua watoto wake wawili kwa kuwanywesha sumu kutokana na msongo wa mawazo amefariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema Daines alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na alifariki dunia Machi 9, 2024 majira ya saa 10:15 jioni.
Amesema, marehemu akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Mashese – Ilungu aliwanywesha sumu ya kuulia magugu aina ya ‘Pare Force’ watoto wake wawili na kusababisha vifo vyao na kisha na yeye alikunywa sumu hiyo ya kuulia magugu iliyopelekea kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa matibabu.
Kamanda Kusaga amewataja watoto hao waliofariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kwa matibab kuwa ni Mario Semen Adamson (4) na mdogo wake wa kike Beonis Semen Adamson (2), wote wakazi wa Mashese.