MICHEZO
Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Klabu za Simba SC, Coastal Union, Mwadui FC na Namungo FC, Jamhuri Kikwelo ‘Julio’ anatajwa kuwa chaguo la kwanza kwa makocha wanaopewa nafasi ya kukabidhiwa majukumu ya kukifndisha kikosi cha Singida Fountain Gate.
Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ipo katika mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya, baada ya kumtimua Kocha kutoka Afrika Kusini Thabo Senong, aliyeondoka na benchi lake lote la ufundi.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema Julio huenda akatangazwa rasmi baada ya kumalizika kwa mchezo wa leo Jumanne (Machi 12) kati ya timu hiyo dhidi ya Simba SC, ambao utaendelea kusimamiwa na Kaimu Kocha Mkuu, Ngawina Ngawina.
Chanzo kinasema Julio amekuwa chaguo la timu hiyo baada ya uongozi wa Singida FG kushindwa kumnasa Juma Mgunda ambaye alikuwa ni chaguo la kwanza.
“Ni kweli tulimtaka Mgunda, hakupatikana, lakini tupo kwenye mazungumzo na Julio, kama tutakamilisha mapema makubaliano tutamtangaza baada ya mechi dhidi ya Simba SC, kilisema chanzo chetu.
Hivi karibuni timu hiyo ilitimua benchi lote la ufundi kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Hussein Massanza, ni kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye Ligi Kuu.
Timu hiyo imecheza mechi nane bila kupata ushindi, ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 27, mwaka jana, ilipoifunga Coastal Union mabao 2-1 nyumbani, na hadi leo hii haijaonja ladha ya ushindi ikicheza mechi nane, ikipoteza tano na sare tatu.
Desemba Mosi, mwaka jana, ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania, na sare nyingine na mechi inayofuata ikatoka suluhu dhidi ya KMC, kabla ya kwenda kukutana na kipigo cha bao 1-0, Uwanja wa Nyankumbu, Geita, dhidi ya Geita Gold.
Ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, kabla ya kupata kipigo kingine cha mabao 3-1 dhidi ya Prisons, na kwenda kutoa sare ya bao 1-1, dhidi ya Tabora United.
Baada ya hapo ikachapwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kabla ya kubamizwa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.