HABARI KUU
Polisi nchini Kenya wamemkamata tena mshukiwa wa mauaji ambaye alitoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi, vimeripoti vyombo vya habari vya Kenya.
Kelvin Kangethe, 41, anatafutwa na mamlaka za Marekani kuhusiana na mauaji ya mpenzi wake mjini Boston mwaka jana.
Kangethe hajasema lolote kuhusu tuhuma hizo.
Alikuwa amekamatwa na mamlaka za Kenya akisubiri uamuzi wa ama kupelekwa Marekani au la, limeripoti Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC.
Wiki iliyopita alitoroka kutoka kituo kimoja cha polisi mjini Nairobi, ambapo alikuwa anashikiliwa.
Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei amesema mshukiwa huyo alikamatwa Jumanne usiku katika eneo la Ngong kwenye viunga vya Nairobi, kufuatia msako wa siku tano.
Polisi walisema Bwana Kangethe alitoroka – kwa kutoka tu- kwenye kituo cha polisi cha Muthaiga alipokuwa akishikiliwa.
Wanasheria wake wamesema maisha ya mteja wao yako hatarini.