HABARI KUU
Waziri wa Maji Mhe Jumaa Hamidu Aweso (Mb), amewasili Paris nchini Ufaransa na kupokelewa na mwenyeji wake Mhe Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Ali Jabir Mwadini kwa mwaliko maalum wa Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (Agence Française de Développement – AFD).
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Aweso atafanya mazungumzo na Mheshimiwa Chrysoula Zacharopoulou, Waziri wa Nchi-Maendeleo ya Uchumi Ufaransa (Secretary of State for Economic Development) pamoja na Uongozi wa Shirika la AFD.
Mazungumzo hayo yatajikita katika uwekezaji na utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria katika Jiji la Mwanza ambapo awamu ya kwanza imetekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank) na Benki ya maendeleo ya Ufaransa (AFD) kwa gharama ya takribani Euro Milioni 135.5
Aidha Waziri Aweso atafanya mazungumzo na Uongozi wa Benki ya Maendeleo AFD ukiongozwa na Marie-Hélène LOISON Naibu Meneja Mkuu wa AFD ambapo kwa pamoja watajadili utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea katika miji ya Shinyanga na Morogoro inayofadhiliwa na Serikali ya Ufaransa kupitia Benki yake ya Maendeleo (AFD) kwa gharama ya Jumla ya Euro 145 milioni.
Vilevile, mazungumzo hayo yatahusu kupanua wigo wa uwekezaji katika Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira katika Ziwa Victoria awamu ya Pili yenye thamani ya Euro Milioni 180.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Aweso atashiriki katika mahafali ya watumishi wa Sekta ya Maji katika chuo cha AgroParsTech kupitia ufadhili wa AFD ikiwa ni pamoja na wakurugezi wa Mamlaka za Maji waliokua wakiongeza ujuzi.
Katika hafla hii inatarajiwa kuwa Mheshimiwa Aweso atafanya mazungumzo ya kuanzisha ushirikiano kati ya AgroParisTech na Chuo cha Maji.