HABARI KUU
Watekaji nyara nchini Nigeria wameomba walipwe Naira Bilioni 1 (pauni 486,000) ili kuweza kuwaachia watu 286 wanaowashikilia.
Kati ya waliotekwa wamo Wafanyakazi pamoja na watoto wa shule, takribani watoto 100 wakiwa na umri kati ya miaka 12 au chini zaidi.
Watu hao walitekwa Alhamisi iliyopita katika mji wa Kuringa Kaskazini Magharibi mwa Jimbo la Kaduna.
Msemaji wa familia za mateka hao Jubril Aminu, amesema kuwa kupitia mazungumzo ya simu watekaji hao walitishia kuwaua mateka na wametaka pesa hizo zilipewe ndani ya siku 20.
Diwani mmoja amethibitisha kuwa watu hao walipiga simu jana kwa nambari isiyojulikana.
Serikali ya Nigeria imeyahimiza Majeshi ya usalama nchini humo kuhakikisha wanawaokoa mateka kwa haraka bila ya kulipa chochote.
Vitendo vya utekaji nyara vimekithiri nchini Nigeria kwani ndani ya wiki moja tu makundi matatu yalitekwa katika maeneo tofauti.