MAKALA
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha miradi mitatu ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 111.4 mkoani Mara.
Miradi hiyo ni ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Nyamuswa – Bunda-Bulamba (km 56.4), Makutano Juu- Sanzante (km 50) pamoja na barabara ya Musoma – Busekela (km 92), kipande cha kwanza cha kutoka Kusenyi – Suguti (km5).
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema hayo Machi 13, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.
“Tunaishukuru serikali yetu chini ya mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 137.165 ili kutekeleza mradi wa barabara hizi tatu ambazo ujenzi wake umekwishakamilika” amesema Mhandisi Maribe.
Amesema kufunguliwa kwa barabara hizo kumeongeza uchumi wa Mkoa kwa kurahisisha usafiri kwa watalii wanaokuja nchini kuelekea Katika mbuga ya Serengeti; pia zimechochea fursa kwa wafanyabishara wa madini kuweza kuuza madini yao katika soko la kimataifa pamoja na kurahisha huduma ya usafiri wa kutoka Mkoa Mara kwenda Mikoa Jirani kwa uharaka zaidi tofauti na hapo awali.
Ametaja miradi mingine inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami kuwa ni Barabara ya Sanzante- Nata (km 40), Mogabiri-Nyamongo (km 25), Tarime-Mugumu (km 87.14) na sehemu ya Tarime-Mogabiri (km 9.3).
Pia ipo ya Nyamongo-Mugumu (km 48.15) na barabara ya Mzunguko ya Mugumu (km 3.6), Ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma, pamoja na ujenzi wa mzani wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo.
Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwajali wakandarasi wazawa kwani miradi yote ya matengenezo ya barabara imefanywa na wakandarasi hao ikiwa ni juhudi za serikali kuwajengea uwezo.