MICHEZO
Ligi Kuu ya NBC Tanzania bara inaendelea tena leo Machi 17, 2024 ambapo vinara wa Ligi hiyo, Young Africans Sc watakuwa na kibarua dhidi ya Wanalambalamba, Azam Fc katika pambano ambalo litatoa picha halisi ya mwelekeo wa mbio za ubingwa.
Wakati Azam FC ikihitaji ushindi ili kurejea nafasi ya pili na kuendelea kuipa presha Yanga waliopo kileleni kutakuwa na mpambano wa kuwania ufungaji bora ambapo kinara Stephanie Aziz Ki (magoli 13) atahitaji kuongeza akaunti yake ya magoli huku Feisal Salu ‘Feitoto’ (magoli 12) naye akihitaji kuweka hai matumaini yake ya kuwa mfungaji bora.
Azam Fc ambao ndio wenyeji wa mchezo huo wanahitaji kufuta uteja mbele ya Wananchi baada ya kuambulia ushindi mmoja tu kwenye mechi 6 zilizopita za ligi kuu, sare moja na vipigo vinne.
Kiujumla Azam FC na Yanga Sc zimekutana mara 31 kihistoria tangu ipande daraja mnamo 2008 huku Wanalambalamba wakishinda mara 9, sare 9 na vipigo 13.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana Yanga ilishinda 3-2 huku ushindi pekee ambao Waoka Mikate wanajivunia dhidi ya Wananchi ni ule wa 1-0 mnamo Aprili 25, 2021 kwa bao pekee la Prince Dube.