HABARI KUU
Rubani mmoja wa Shirika la Ndege la Delta, amehukumiwa kifungo cha miezi 10 Jela kwa kufika kazini akiwa amelewa.
Mnamo Juni 16 mwaka jana Rubani Lawrence Russell Jr (63) raia wa Marekani alikuwa akijiandaa kurusha Ndege kutokea Edinburgh, Scotland kuelekea New York, Marekani.
Baada ya vipimo vya kawaida kabla ya kuanza safari, Rubani huyo alikutwa na kiasi cha pombe kwenye damu kilichozidi kikomo cha kisheria.
Aidha, rubani huyo alikutwa na chupa mbili za pombe kali aina ya ”Jägermeister” kwenye begi lake, huku chupa moja ikiwa wazi na imebaki nusu. Kinywaji hicho kina kiasi cha pombe cha asilimia 35.
Kwa mujibu wa nyaraka kutokea Mahakama ya Scotland, safari ya Ndege aliyokuwa akitakiwa kuiongoza ilifutwa na Rubani Russell alifukuzwa kazi.
Mahakama hiyo imesema Russel alikuwa mlevi aliye kwenye matibabu, na alishawahi kukamatwa mara mbili akiendesha gari huku akiwa amelewa.
Baada ya tukio rubani huyo wa Boeing 767 amefanikiwa kumaliza programu ya matibabu ya ulevi.
Russel alikiri kosa mnamo Machi 5 kitendo kilichomfanya kupunguziwa hukumu kutokea miezi 15 hadi miezi 10.