MICHEZO
Kocha Mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps amesema kukosa nafasi ya mara kwa mara ya kucheza kwa Mshambuliaji Kylian Mbappe kwenye klabu yake ya Paris Saint-Germain ni habari njema kwa timu ya taifa ya nchi hiyo.
Nahodha huyo wa Ufaransa aliiweka wazi PSG mwezi uliopita kwamba ataondoka kwenye klabu hiyo pindi mkataba wake utakapofikia kikomo mwishoni mwa msimu, uamuzi uliofanya staa huyo kucheza dakika 90 kwenye mechi tatu tangu Februari 14.
Mechi hizo ambazo Mbappe alimaliza dakika 90 ni dhidi ya Real Sociedad ambapo PSG walishinda mabao 2-1, ushindi wa mabao 2-1 kwenye Kombe la Ufaransa dhidi ya Nice na ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Montpellier, mwishoni mwa juma lililopita (Jumapili-Machi 17).
Alipoulizwa kuhusu kukosa muda wa kucheza kwa nyota huyo, Deschamps aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Ni muhimu kwa mchezaji kuwa fiti kimwili kwa ajili ya mashindano makubwa. Kwa namna yoyote ile, wachezaji watakaokuwa wanatumika mara kwa mara watafika mwisho wa msimu wakiwa wamechoka kidogo.
“Kama hali hiyo ya uchovu inaweza kupungua kidogo ni vizuri zaidi,” alisema kocha huyo kuelekea mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ujerumani Machi 23.
Mbappe ambaye anahusishwa na kujiunga na klabu ya Real Madrid mwishoni mwa msimu, amesema ana matumaini ya kushiriki kwenye michuano ya Olimpiki itakayofanyika Ufaransa mwaka huu.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.