MICHEZO
Mahakama ya Hispania imesema mlinzi wa zamani wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Dani Alves anaweza kuachiwa huru baada ya kutumikia Robo ya adhabu yake ya ubakaji.
Alves, aliyehukumiwa kifungo cha miaka minne na nusu jela mwezi uliopita, anaweza kuachiwa huru akilipa euro milioni moja ambazo ni sawa na Pauni 853,000. Aliwekwa kizuizini tangu Januari mwaka 2023.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 40 alikutwa na makosa ya kubaka kwenye klabu ya usiku Desemba mwaka 2022, Barcelona. Wakili wa mwathirika aliuita uamuzi huo kuwa ni kashfa.
Moja ya masharti ya kuachiwa huru kwa nyota huyo ni kukabidhi pasipoti zake za Hispania na Brazil.
Anatakiwa kuonekana mahakamani kila wiki. Masharti mengine ni mtuhumiwa kutomsogelea mwathirika.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya mawakili wa Alves kuomba mteja wake aachiwe huru kwa sababu tayari ameshatumikia robo ya kifungo chake kufuatia kuwekwa kizuizini alipokamatwa awali.
Wakili wa mwathirika, Ester Garcia, alisema: “Kwangu, ni kashfa kumruhusu ambaye wanajua anaweza kupata mamilioni ya euro kuwa huru.”
Garcia alisema amechukizwa na uamuzi huo wa mahakama, na kuongeza ni mfumo wa utoaji haki unaowapendelea matajiri na kwamba atakata rufaa.