MICHEZO
Beki wa Newcastle United, Sven Botman anatarajia kukaa nje ya dimba kwa kipindi cha miezi nane kufuatia kupata majeraha ya goti.
Raia huyo wa Uholanzi, alipata majeraha mwishoni mwa juma lililopita katika mchezo wa Kombe la FA kati ya timu yake dhidi ya Manchester City na baadaye kulazimika kutolewa nje.
Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 24, anatarajia kufanyiwa upasuaji juma lijalo baada ya vipimo kukamilika.
Taarifa iliyotolewa katika mtandao wa klabu ilisema, Botman amepata majeraha makubwa na kwamba atakaa nje ya dimba kwa muda mrefu.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba, watamkosa mchezaji huyo muhimu kikosini kwani majeraha yatamweka nje ya dimba muda mrefu, lakini wana imani atarejea dimbani mapema.
“Kila mmoja wetu katika kikosi cha Newcastle amesikitishwa majeraha aliyoyapata Botman katika kipindi ambacho anahitajika kwani ni mmoja wa wachezaji muhimu kikosini.”
“Tunamwombea apone mapema na kurudi katika hali yake ya kawaida kwani ni mchezaji muhimu kwetu,” ilisema taarifa hiyo.
Botman awali alipata majeraha ya goti Septemba, mwaka jana yaliyomweka nje va dimba kwa muda na kuzikosa mechi 17 zikiwemo tano za mwisho za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kurudi Desemba, mwaka jana.
Botman ameanza mechi nyingi tangu arejee dimbani Desemba mwaka jana, lakini alilazimika kutolewa nje dakika ya 83, katika mchezo waliopoteza mabao 2-0 dhidi ya Manchester City.