MICHEZO
Mlinda Lango wa Real Madrid, Thibaut Courtois amefanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia alioumia kwenye zoezi ya timu hiyo juzi Jumatano (Machi 20).
Mlinda mlango huyo wa zamani wa klabu za Atletico Madrid na Chelsea, atakuwa nje ya uwanja kwa majuma kadhaa kutokana na majeraha hayo aliyoyapata Jumanne (Machi 19).
“Courtois ataanza mchakato wa kuuguza majeraha yake katika siku zijazo,” ilisema taarifa ya Madrid.
Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 31 alitazamiwa kurejea kwenye kikosi cha miamba hiyo ya soka ya Hispania baada ya kutumia miezi kadhaa nje ya uwanja akiuguza majeraha yake aliyoyapata Agosti mwaka jana.
Courtois ambaye pia ni kipa chaguo la kwanza kwenye timu ya taifa ya Ubelgiji, aliichezea Madrid mechi 31 msimu uliopita, lakini bado haijatumikia hata mchezo mmoja timu hiyo msimu huu 2023/24.
Madrid, inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania kwa tofauti ya alama nane dhidi ya wapinzani wao wakubwa FC Barcelona, itaikaribisha Athletic Bilbao Machi 31.