HABARI KUU
Mwanafunzi wa kidato cha tano, Frank Matage kutoka Shule ya Sekondari Kemebos, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera amefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa katika ajali ya basi mali ya shule hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amesema kuwa ajali hiyo imehusisha gari la wanafunzi wa Shule ya Kemibos lenye namba za usajili T 770 DSQ, lililokuwa likisafiri kutoka Bukoba kuelekea Mkoa wa Geita kurejesha wanafunzi nyumbani baada ya shule kufungwa kwa ajili ya likizo fupi.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa nane katika Kata ya Kimwani, wilayani Muleba ambapo jumla ya wanafunzi 35 walikuwa ndani ya gari hiyo.
Amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye alishindwa kukata kona.
Akizungumzia hali za majeruhi hao sita, Dk Nyamahanga amesema, wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba.
Aidha, amewataka madereva wa vyombo vya moto nchini kuendesha kwa tahadhari hasa wanapoendesha majira ya usiku ili kuweza kudhibiti uwepo wa ajali katika wilaya hiyo.