HABARI KUU
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema uamuzi wa kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar ulizingatia kutanguliza mbele usalama wa maisha ya watu, maslahi, utulivu na mstakabali mwema wa Zanzibar, Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla, kuliko vyama vya siasa.
Balozi Dk. Nchimbi amesema uwepo wa Serikali hiyo Zanzibar umeondoa hali ya siasa za chuki na uhasama mkubwa uliokuwepo kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuundwa kwake, huku akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa uongozi kwa nchi ili kudumisha umoja na utulivu uliokusudiwa kwa maslahi ya Wazanzibar na Watanzania wote.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akizungumza na Wazee wa Zanzibar, Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, leo Jumapili, Machi 24, 2024, ikiwa ni siku ya pili akiwa kwenye ziara ya kikazi.
“Binafsi nikimsikia mtu anazungumzia kutaka kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, simwelewi huyo mtu hata kidogo. Kwa sababu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa kwa ajili ya usalama wa maisha ya watu, usalama wa Wazanzibar, usalama wa Watanzania. Maisha ya watu ni muhimu sana kuliko kitu chochote kwanza. Tuliweka mbele maslahi ya nchi, utulivu na umoja wetu, si vyama vya siasa.
“Mnakumbuka wakati fulani nikiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kila siku nenda rudi kwa helkopita kuja Zanzibar. Tulikuwa tunahangaika kuondosha uhasama na chuki. Najua kuna wakati wenzetu wanapata gadhabu na kuzungumza kwa jazba. Sisi wanaCCM tusiende huko hata kidogo. Sisi ndiyo Chama tawala. Sisi ni walezi. Mlezi hasusi. Tusiache wajibu wetu wa kulea hata kidogo. Mtoto ndiye anasusa. Na katika hili naombeni sana wazee wote wa Zanzibar na Tanzania, mniunge mkono,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.
Aidha, Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Nchimbi pia amesisitiza msimamo wa CCM kuendeleza kutimiza wajibu wa kipekee wa kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na misingi yake.