HABARI KUU
Ndege mpya ya abiria aina ya Boeing B737-9 Max ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) inatarajiwa kuwasili nchini, huku Watanzania na viongozi mbalimbali wakialikwa kwenda kushuhudia mapokezi hayo.
Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 181 itawasili nchini kesho kuanzia saa 04:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA).
Akizungumzia ujio wa ndege hiyo inayotokea Marekani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuwasili kwa ndege hiyo ni muendelezo wa Serikali katika jitihada za kuboresha sekta ya uchukuzi ili kukuza uchumi wa nchi.
“Ujio wa ndege hii ni alama ya ushindi kwa Taifa, na fahari kubwa hivyo nichukue fursa hii kuwaalika wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Watanzania wote kuja kushiriki mapokezi ya ndege hii kuanzia saa 10:00 Asubuhi Terminal one katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” amesema Chalamila
.
Chalamila aliyezungumzia maandalizi ya mapokezi hayo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema aina hiyo ya ndege ni ya pili kuwasili nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi 19,2021.
“Tulipokea Ndege ya kwanza ilikuwa ya abiria, ikaja ya mizigo na sasa hivi ni ndege ya tatu ya abiria lakini ni ya pili kwa aina ya Max,” amesema Chalamila.
Kuongezeka kwa ndege hiyo kunalifanya shirika hilo kufikisha jumla ya ndege 14; kati ya hizo moja ni ya mizigo na zinazobakia zinabeba abiria.