NYOTA WETU
Simba SC inakamilisha mazungumzo na beki wa kushoto mmwaga maji wa Al Hilal, Ibrahim Imoro anayesifika kwa kukaba na kupandisha timu na kupiga krosi za maana kwa washambuliaji.
Chanzo makini kutoka ndani ya Simba SC kinasema beki huyo kutoka nchini Ghana anatakiwa kutua Msimbazi ili kuja kusaidiana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa muda mrefu hana mbadala kikosini katika eneo hilo la kushoto.
Imoro anayemudu pia kucheza kama winga wa kushoto, kwa sasa yupo huru baada ya kuvunja mkataba na Al Hilal iliyomsajili Agosti 5, 2022 kutoka Asante Kotoko ya Ghana tangu Julai mwaka jana na tayari ameshaanza mazungumzo na mabosi wa Msimbazi ili aje kuitumikia msimu ujao.
Mghana huyo mwenye umri wa miaka 24 amewahi kutwaa Tuzo ya Mchezaji aliyeasisti mabao mengi katika Ligi ya Ghana msimu wa 2021-2022 akitoa pasi tisa, pia ametwaa mataji zaidi ya manne ikiwamo la Ligi Kuu Ghana akiwa na Asante Kotoko msimu wa 2021-2022 na Kombe la Rais (Ghana) 2019 na taji la Sudan Super Cup 2022 akiwa na Al Hilal.