HABARI KUU
Rais wa Senegal anayemaliza muda wake, Macky Sall amempongeza mgombea wa upinzani, Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi alioupata huku mshindani wake wa karibu, Amadou Ba akikubali kushindwa katika uchaguzi huo.
Baada ya mgombea huyo wa chama tawala, Amadou Ba kutambua ushindi wa Faye katika duru ya kwanza na kutoa pongezi zake, Sall, ambaye alishinda chaguzi za mwaka 2012 na 2019, amesema “napongeza maandalizi mazuri ya uchaguzi na nampongeza mshindi, Bassirou Diomaye Faye ambaye mwenendo wa kura unaonyesha kwamba ameshinda.”
Mgombea huyo wa upinzani aliyeshinda hajawahi kushika nafasi ya kuchaguliwa ya kitaifa na bado hajazungumza hadharani tangu uchaguzi wa Jumapili Machi 24, 2024, uliofuatia miaka mitatu ya machafuko na mgogoro wa kisiasa.
Mpinzani wake mkuu kutoka muungano wa chama tawala, Amadou Ba ametambua ushindi wa Faye katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na akatoa pongezi zake, ilisema taarifa.