MICHEZO
Kikosi cha Mamelodi Sundowns ambacho kinatarajiwa kutua nchini kesho Jumatano (Machi 27) kitakuwa bila nahodha wake Themba Zwane, ambaye hatacheza mchezo wa Jumamosi (Machi 30).
Mamelodi itatua nchini na zaidi ya watu 70 kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Young Africans, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa 3:00 usiku.
Zwane ambaye ni mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho hatakuwepo kwenye mchezo huo baada ya kuwa na kadi tatu za njano alizopewa kwenye mechi za hatua ya makundi.
Huyu ni kati ya mastaa wa Mamelodi ambao wamekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho alichoanza kukitumikia mwaka 2011, lakini akiwa na historia nzuri ya kupewa kadi kwenye michezo ya ligi pamoja na ile ya kimataifa.
Kiungo huyo mshambuliaji, alipewa kadi kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe katika dakika ya 47, Pyramids dakika ya 65 na kurudia tena kwenye mechi dhidi ya Mazembe dakika ya 90.
Rekodi zinaonyesha kuwa kiungo huyo anayeichezea timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ alijiunga na Mamelodi mwaka 2011.
Kwenye michezo sita ya makundi amecheza dakika 328, lakini akitajwa kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho, mara nyingi amekuwa akikosekana kwenye kikosi cha Mamelodi anaingia winga Lesiba Nku.
Zwane anayevaa jezi namba 18, ameitumikia Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ kwenye michezo 39 na kufunga mabao tisa, akiwa kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu amepiga pasi 222, amegusa mpira mara 322, hajafunga bao lolote, akipiga mashuti manne na mawili ndiyo yamelenga lango.
Kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’, alifunga mabao mawili kwenye michezo ya hatua ya makundi.