HABARI KUU
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kukuza uchumi wa sekta binafsi inayochangia makusanyo ya kodi ambazo zitawezesha ujenzi wa miundombinu ya barabara na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.
Bashungwa amezungumza hayo leo katika kikao kilichowakutanisha wafanyabiashara wa wilaya ya Karagwe pamoja na taasisi za Serikali zinazowahudumia ambapo amesikiliza kero zao ikiwemo tozo kubwa za kodi, ushuru pamoja na kauli zisizoridhisha kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Sijafurahishwa na madai ya kauli za maafisa kwa wafanyabiashara ambazo sio sahihi, kwa kuwaambia wakishindwa kulipa kodi, wafunge biashara. Lengo la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha kwa kutoa elimu, kuwashauri na kustawisha wafanyabiashara,”
amesisitiza Bashungwa.
Aidha, ameutaka uongozi TRA Mkoa wa Kagera kusimamia miongozo pamoja na kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za kodi mara kwa mara kwa wafanyabiashara pamoja na maafisa kuwa na kauli nzuri na wezeshi.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Omary Kigoda amesema suala la lugha mbaya kwa walipa kodi sio msimamo wa taasisi, hivyo TRA itaendelea kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.