MICHEZO
Waendesha mashtaka nchini Uhispania wametaka aliyekuwa Rais wa Shirikisho la soka la nchi hiyo Luis Rubiales afungwe jela kwa miaka miwili na nusu kwa kosa la kumbusu mchezaji wa kike bila ridhaa yake.
Tukio hilo lilitokea mwezi Agosti mwaka jana wakati Uhispania ilipokuwa ikisheherekea ushindi katika fainali za Kombe la dunia la Wanawake.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, Mwendesha Mashtaka Marta Durantez amemshtaki Rubiales kwa kosa la unyanyasaji wa kijinsia, kulazimisha busu kwa mchezaji, pamoja na matendo yake baada ya tukio.
Vilevile Mwendesha Mashtaka huyo amemtuhumu kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Uhispania Jorge Villda, Mkurugenzi timu Albert Luque, na Mkuu wa kitengo cha mauzo cha Shirikisho Ruben Riviera kwa makosa ya kumlazimisha Bi.Hermoso kusema kuwa aliridhia kupigwa busu lile.
Watatu hao wamekana tuhuma hizo. Ikiwa watakutwa na hatia, watahukumiwa kifungo cha miezi 18 jela.
Mwendesha Mashtaka amewataka watuhumiwa kwa pamoja kumlipa Bi.Hermoso fidia ya jumla ya dola za kimarekani 100,000. Katika kiasi hiko Rubiales atatakiwa kulipa angalau nusu nzima.
Vilevile Bi.Durantez ameomba uwekwe utaratibu wa kizuizi kitakachompiga marufuku Rubiales kumsogelea Bi.Hermoso kwa mita 200, na kutowasiliana naye kwa miaka saba na nusu ijayo.