HABARI KUU
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma (81) amenusurika kwenye ajali ya gari iliyotokea jana jioni katika jimbo la KwaZulu Natal.
Katika ajali hiyo mtu mmoja aliyekuwa akiendesha gari huku akiwa amelewa aligongana na gari rasmi la serikali lililokuwa limembeba Zuma pamoja na timu yake rasmi ya ulinzi.
Kwa mujibu wa polisi, watu wote walitoka salama na mwanasiasa huyo mkongwe alitolewa na kupelekwa nyumbani. Aidha mtu mmoja amekamatwa kwa uzembe uliopelekea ajali hiyo.
Kiongozi wa uchaguzi katika chama cha uMkhonto we Sizwe (MK) ambacho Zuma amekuwa akipigia kampeni, amedai kuwa ajali hiyo ilikuwa ikimlenga Zuma.
Mapema jana, tume ya uchaguzi ilitangaza kumzuia Zuma kugombea katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajia kufanyika Mei 29.